Wednesday, June 18, 2014

Idadi Ya Watumiaji Na Waathirika Wa Dawa Za Kulevya Inatajwa Kuendelea Kuongezeka

Idadi ya Watumiaji na waathirika wa Dawa za kulevya inatajwa kuendelea kuongezeka nchini huku kukiwa na mshituko mkubwa kutokana na matumizi ya dawa hizo kupenya kwa kasi hadi maeneo ya Vijijini.
Hali ni mbaya zaidi kwa Jiji la Dar es salaam ambapo katika kipindi cha mwezi Mei mwaka huu Watumiaji wa Heroin wanaopata tiba ya methadone katika Hospitali za Jiji la Dar es salaam wamefikia 1,526.
Matumizi ya Dawa hizo yanaelezwa  kuwa na madhara mengi kiafya na kijamii ikiwemo kudhoofisha afya za Watumiaji na kuathiri uwezo wao wa kufanya kazi  pamoja na kukumbwa na magonjwa mbalimbali yakiwemo ya akili, homa ya ini, moyo mapafu na kifua kikuu.
Hali hiyo inawagusa Viongozi wa Dini ambao wanaamua kukutana na kujadili juu ya namna ya kukabiliana na tatizo hilo kutokana na nafasi waliyonayo katika jamii.
Wakati Viongozi hao waandamizi wa Dini wakieleza hayo baadhi ya Washiriki wa Mkutano huo wanaeleza kusikitishwa na ongezeko la Watumiaji na waathirika wa Dawa za Kulevya nchini akiwemo Mchungaji CHRISTOPHER KALATE wa KKKT Dayosisi ya Pwani na Sheikh ASIF MUYENGA kutoka Taasisi ya Daarul Muhibi.
Kwa Jiji la Dar es salaam hali inaelezwa  kuwa mbaya zaidi kwa Manispaa ya Ilala.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam ambae pia ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala, RAYMOND MUSHI amekiri kuwepo kwa tatizo hilo katika Wilaya yake na kubainisha Mikakati iliyowekwa  kulipatia ufumbuzi tatizo hilo.
Kiwango kikubwa cha Dawa za Kulevya zinazoingizwa nchini kupitia Barabara, Bandari na Viwanja vya Ndege zinaletwa kutoka nchi za nje.
Katika Kipindi cha Mwezi Januari, mwaka 2013 hadi Mwezi Mei, mwaka huu Kikosi cha Kupambana na Dawa za Kulevya nchini kimefanikiwa kukamata zaidi ya kilo 98 elfu za dawa za kulevya .

No comments:

Post a Comment