Polisi nchini
Kenya wamesema kuwa wamewakamata washukiwa wawili wa mashambulizi yaliyofanyika
mjini Mpeketoni, Pwani ya Kenya na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 60.
Kundi la
wapiganaji wa Al Shabaab limekiri kufanya mashambulizi hayo yaliyofanyika
Jumapili usiku na Jumatatu usiku ingawa serikali ya Kenya imesema kuwa
mashambulizi hayo yalichochewa kisiasa.
Rais Uhuru
Kenyatta katika hotuba yake kwa taifa, amelaumu vikundi vya wanasiasa pamoja na
makundi ya watu ambayo yana nia ya kufaidi kutokana na hali mbaya ya usalama
nchini humo kwa kufanya mashambulizi hayo.
Maafisa
kadhaa wa polisi wa eneo la Mpeketoni, wamefukuzwa kazi na wengine kuhamishwa
kutoka vituo vyao vya kazi katika eneo hilo.
Hii ni
baada ya tuhuma dhidi yao kuwa walipuuza onyo la kutokea kwa mashambulizi hayo
kutoka kwa shirika la ujasusi na Wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu
mashitaka.
No comments:
Post a Comment