Friday, May 2, 2014

BOB MARLEY: MWANAMUZIKI WA KWANZA TAJIRI DUNIANI TOKA NCHI ZA DUNIA YA TATU (THIRD WORLD COUNTRIES)

Inakadiriwa utajiri wa Bob Marley hadi kufikia mwishoni mwa  2013 unafikia dola milioni 18, na kumfanya kuwa mwanamuziki wa kwanza tajiri kati ya wanamuziki wanaotoka nchi za dunia ya tatu licha ya kuwa amefariki toka mwaka 1981. Pia Bob Marley anashika namba tatu duniani kati ya wanamuziki matajiri ambao ni marehemu, Michael Jackson akiongoza kwa utajiri wa dola milioni 160, wa pili ni Elvis Presley dola milioni 55.

Bob Marley alizaliwa tarehe 6 February 1945 huko kijijini
Nine Mile, Saint Ann, Jamaica. Maisha yake utotoni yalikuwa kama maisha ya watoto wa vijijini huko Jamaica, maisha ya kuchunga na kukamua maziwa mifugo, kwenda bustanini kulima mboga, n.k. Kitu kikubwa alichokuwanacho Bob ni mapenzi makubwa kwa muziki. Aliweza kujifunza muziki utotoni hukohuko kijijini kwake hadi anahamia mjini Kingstone alikuwa tayari ana ufahamu wa muziki, ila alipata ujuzi zaidi alipokuwa Kingstone, maana eneo alilokuwa anaishi na mama yake hapo Trenchtown ndio palikuwa ni kitovu cha vipaji vyote toka muziki hadi michezo visiwani Jamaica. 

Historia ya mafaninikio ya Bob Marley inaanzia mwaka 1973 pale walipokwama kifedha nchini Uingereza walipokwenda kufanya maonyesho akiwa na wenzake Peter Tosh na Bunny Wailer wakiwa na kundi zima la The Wailers kushindwa kuvuta mashabiki wengi kwenye maonesho yao na hatimaye kukosa pesa za kuwarudisha Jamaica. 

Waanzilishi wa kundi la muziki wa reggae The Wailers, Peter Tosh Bunny Wailer na Bob Marley
Wakiwa bado nchini Uingereza wakitafuta njia ya kujikwamua waweze kurudi kwao Jamaica walibahatika kukutana na Chris Blackwell mmiliki wa lebo ya Island records, baada ya mazungumzo na The wailers aliwapa mkopo wa paundi 4,000 ya Uingereza kwa makubaliano ya Bob na wenzake wakarekodi nyimbo na kurudi na nyimbo hizo Island records kwa ajili ya kutoa album.

Chris Blackwell na Rita Marley
Waliporudi Jamaica, The Wailers walifanikiwa kurekodi nyimbo zaidi ya tisa. Bob Marley aliporudi Uingereza na kumkabidhi Chris Blackwell tepu ya nyimbo zao producer huyo alizichagua nyimbo 9 na  kuzifanyia kazi nyimbo hizo, kati ya nyimbo hizo tisa, mbili zilitungwa na Peter Tosh na saba Bob Marley. Mnamo tarehe 13 April, 1973 album ya Catch a Fire ilitoka rasmi. Chris Blackwell alifanya juhudi kubwa kuitangaza album hii ya reggae na kundi la Wailers huko Uingereza na Marekani. Mwaka 1974 Peter na Bunny waliondoka toka kwenye bendi yao The Wailers na kumuacha Bob Marley peke yake kati ya waanzilishi wa bendi yao.

Bob Marley aliisuka upya bendi aliwaingiza wanamuziki wapya na wazamani pia walikuwepo, wanamuziki hao ni pamoja na ndugu Calton Barrett (drums) na Aston "family man" Barrett (Bass guitar), Junior Marvin na Al Anderson (Lead guitar), Tayrone Downie na Earl Lindoon (Keyboards) na Alvin "Seeco" Patterson (percussions). wakina dada watatu pia walikuwapo kama waimbaji waitikiaji The I Three hawa ni pamoja na Juddy Mowatt, Marcia Griffiths na mke wa Marley, Rita. wanabendi hawa kwa pamoja walijulikana kama "Bob Marley and The Wailers"   


Bob Marley na kundi lakeThe Wailers
Mmoja kati ya wanamuziki aliyewahi kufanya kazi na Bob (Marcia Griffiths) katika mahojiano na mwandishi wa habari alizungumzia juu ya safari ya kimuziki ya kundi lao haikuwa rahisi maana alishuhudia walipokuwa wakipiga huku wapenzi wakiwa katika mamia, baadae idadi ikawa inaongezeka kufikia maelfu, elfu kumi, elfu themanini hatimae waliweza kuwa na uwezo wa kukusanya hadi wapenzi zaidi ya laki moja kwenye maonesho yao.

Baada ya hali kuwa nzuri Bob Marley alinunua nyumba iliyokuwa inamilikiwa na Chris Blackwell, nyumba hiyo ilikuwa katika eneo la watu mashuhuri na matajiri kisiwani Jamaica. Kununua kwa nyumba hiyo kulimfanya Bob kuwa rastafari wa kwanza kutoka maisha ya gheto kuja kumiliki nyumba maeneo ya matajiri.  

Bob Marley akiwa katika moja ya maonesho yake ya muziki

Nyumba hiyo ya Bob Marley ilikuwa kama ni makao makuu ya marasta, watu wa aina mbalimbali kutokea maeneo mengine ya Kingston walikuwa wakifika hapo 56 Hope Road kuongea na kujadiliana mambo mbalimbali, toka habari za siasa, historia, michezo mpaka habari za dini, kwa ujumla kulikuwa na kila aina ya mijadala hapo.

Bob alikuwa mkarimu sana kwa watu waliokua wakifika hapo kwake, aliwakarimu juisi, chai, samaki na kila alichoweza kuwapa wageni wake. Pia aliwasaidia watu wengi sana kwa pesa kwa wale waliokua na shida. Bob alikuwa akipenda kuona watu wanafuraha.

Bob Marley akisakata kabumbu
  
BAADHI YA KUMBUKUMBU MUHIMU ZA BOB MARLEY:

Onyesho lake la kwanza kufanya barani Afrika ilikuwa Gabon mwaka 1979.

Mwaka 1980 kwenye sherehe za uhuru wa Zimbabwe aligharamia usafiri kwenda na kurudi kwa wanamuziki na vyombo vya muziki toka Jamaica na UK hadi Zimbabwe.

Bob Marley alipata kuzungumza katika moja ya mahojiano, kitu kimoja angependa kitokee hapa Duniani ni kuona binadamu wa rangi zote wakiishi pamoja kwa upendo bila kubaguana.

Tarehe 22 Aprili 1978 alitumbuiza kwenye onesho la amani na kuwakutanisha na kuwashikanisha mikono stejini wapinzani wakubwa wa kisiasa huko Jamaica Michael Manley na Edward Seaga. Onesho hilo lilikuwa kubwa sana kuwahi kufanyika Jamaica.

Bob Marley akiwa na wanasiasa wapinzani kisiwani Jamaica Michael Manley kushoto na Edward Seaga kulia siku ya onesho la amani
Katika maisha yake kimuziki Bob alikuwa na hamu kubwa  sana kuwakamata mashabiki waafrika huko Marekani. Mashabiki wakubwa wa Bob walikuwa wazungu, maonesho aliyokua akifanya Marekani yalikuwa yanajaza wazungu na waafrika wachache. Hali hiyo ilikuwa inamuumiza sana. 

Katika kujaribu kuleta mageuzi ili apate mashabiki wengi waafrika huko Marekani ilibidi achukue maamuzi magumu, kwa kukubali kutumbuiza kama bendi msindikizaji katika onesho la kundi la muziki la Commodores (kiumashuhuri Bob Marley and the Wailers walikuwa juu zaidi ya Commodores, na ilitakiwa iwe kinyume chake, Commodores kufungua onesho la kundi la Bob Marley)

Bob Marley na kundi zima la Commodores 1980

Kwa kukubali kufanya onesho hilo kabla ya Commodores, muandaaji alifanya mipango ya kundi la Wailers kupata muda mwingi wa nyimbo zao kusikika hewani miezi mitatu kabla ya onesho hilo toka kwenye vituo vya radio jijini New York ambavyo wasikilizaji wake wengi ni Waafrika.

Onesho lilifanyika 20 Septemba 1980 Madison Square Garden, New York. Siku hiyo ya onesho ilikuwa historia mpya kwa milango ya muziki wa reggae kufunguka Marekani baada ya kundi kubwa lililojitokeza la washabiki Waafrika kumkubali rasmi Bob na kundi lake na muziki wake wa reggae.

Mara baada ya onesho la New York, Bob na kundi lake la Wailers walikua na onesho linalofuata huko Pittsburgh, Pennsylvania. Kabla ya onesho hilo Bob aligundulika kuwa na kansa, Bob alipata huzuni kubwa baada ya kubaini asingeweza kupona ugonjwa huo.

Wakati wa majaribio kabla ya onesho (sound check) Bob na kundi lake walitumia zaidi ya masaa mawili kufanya sound check kwa wimbo mmoja tu " I'm Hurting Inside" siku ya onesho 23 Septemba 1980 Bob Marley alifanya onesho lake la mwisho akiwa stejini na kundi lake The Wailers. 

Picha ya nyuma kwenye kava la albamu ya mwisho ya Bob Marley na Wailers, Uprising.


Bob Marley akitumbuiza onesho lake la mwisho 23 Septemba 1980
 Bob Marley alifariki 11 Mei 1981, Miami, Florida. Alizikwa kijijini kwake alikozaliwa, Nine Mile, Saint Ann, Jamaica.

No comments:

Post a Comment