Wednesday, April 30, 2014

MEI MOSI SIKU YA WAFANYAKAZI DUNIANI: HONGERA WAFANYAKAZI

Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani daima yanatukumbusha juu ya harakati za wafanyakazi wakati ule wa karne ya 19 ambapo kulikuwa na mapinduzi ya viwanda 
huko Barani Ulaya. Mapinduzi yaliyosababishwa ukandamizaji mkubwa wa haki za wafanyakazi zikiwa ni pamoja na malipo ya mishahara duni, mazingira duni ya kufanyia kazi, ukosefu wa vitendea kazi bora, kufanya kazi kwa masaa mengi bila ya kufidiwa na mambo mengi kama haya. Wafanyakazi waliteseka na kudhalilika sana hata wakafikia kutafuta njia ya kujinasua kutokana na hali hiyo. 

Wafanyakazi wakiwa katika maandamano ya Mei Mosi 
Kutokana na hali yao duni, njia pekee waliyoiona kuwa itawakomboa ni kuungana pamoja na kupigania haki zao. Walitambua kuwa mtu peke yake hana nguvu mbele ya mwajiri, lakini umoja wao uliwapa ujasiri wa kuwakabili waajiri hao kupitia umoja wao na hatimaye vyama vyao vya wafanyakazi walivyoviunda. 



WAJAWAZITO WALALA SAKAFUNI HOSPITALI YA MAFINGA

AKINAMAMA wajawazito wanaofika kupata huduma katika Hospitali ya Mafinga iliyopo Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, wanalazimika kulala Sakafuni, kutokana na  Uhaba mkubwa wa vitanda unaoikabilii Hospitali hiyo.

Wakizungumzia adha wanayoipata, wajawazito hao wamesema tatizo la vitanda linawafanya baadhi yao kulala watatu katika kitanda kidogo ambacho ni cha mgonjwa mmoja.

Maula Kifwe amesema hali hiyo kwake inamsumbua kwani kila asubuhi amekuwa akiumwa mgongo, na hivyo kuwa na hofu juu ya tatizo hilo ambalo hakutokanalo nyumbani wakati anakwenda kupata huduma katika Hospitali hiyo.

Naye Anna Ngalalekumtwa amesema hali walizonazo za ujauzito, na mbanano uliopo katika wodi ya Hospitali hiyo, ni hatari kwa viumbe vyao vilivyopo tumboni, kwani kitanda wanacholalia wagonjwa watatu ni kidogo na kinastahili kulala mjamzito mmoja pekee.

Pelida Mkakanzi naye amesema hali hiyo inasababisha baadhi ya vichanga kuanguka na hivyo kuwa katika hatari ya kupata ulemavu watoto hao, kwani uangalizi unakuwa mdogo kutokana na mbanano uliopo.

“Madhara tunayoyapata hapa yanayoonekana ni zaidi ya yake yasiyonekana, kwa maana hapa tunapata maradhi ya kuambukizana, jambo ambalo ni hatari, lakini ni hatari zaidi kwa watoto wachanga, kama unavyoona tumebanana hivi, na sisi ni wajawazito, kweli tunaiomba  serikali itusaidie vitanda, maana hii ni hatari kubwa sana,” Walisema.

Akitoa taarifa za changamoto zinazoikabiri Hospitali hiyo, katika uzinduzi wa wodi ya wazazi na watoto wachanga, Mganga mkuu wa Hospitali hiyo ya mafinga Dr. Eugene Lutambi amesema tatizo lililopo ni uhaba wa vitanda kwani jengo hilo linahitaji jumla ya vitanda 80 ili kukidhi mahitaji ya wajawazito.

Dr. Lutambi amesema zaidi ya shilingi Milioni 800 (mianane)  zinahitajika kwa ajili ya kununuliwa vifaatiba, vikiwemo vitanda, ili kukamilisha huduma za uzazi katika wodi hiyo mpya iliyogharimu jumla ya shilingi Milioni 302.

Pia Dr. Lutambi amesema changamoto iliyopo ni msongamano wa akinamama wajawazito wodini, ambao wanalazimika kulala zaidi ya mmoja katika kitanda kimoja na kuwa kuna kipindi wengine hulala chini.

Amesema wodi ya awali ilikuwa ni ndogo zaidi ambayo ilikuwa na uwezo wa kuchukua vitanda 28 pekee, na kuwa kukamilika kwa jengo hilo ni msaada mkubwa utakaopunguza mrundikano wa wagonjwa na hivyo wahudumu kufanya kazi katika mazingira bora.

Hata hivyo amesema licha ya kukamilika kwa jengo hilo bado tatizo la upungufu wa vitanda linabaki pale pale, kwani vitanda vilivyowekwa katika jengo hilo jipya ni vile vilivyokuwa katika wodi nyingine.

Amesema wodi hiyo yenye uwezo wa kulaza wajawazito 60 hadi 80 licha ya kukabiliwa na uhaba wa vitanda, pia halina vifaatiba jambo linalokwamisha utoaji wa huduma bora ambazo zimekusudiwa.

Na kuwa ..."Jengo hili linachumba cha upasuaji (Theatre), chumba cha akinamama wanaosubiri kujifungua (Antenatal room),  chumba cha akinamama ambao tayari wamejifungua (Postnatal room),  chumba kwa ajili ya watoto waliozaliwa kabla ya muda (Premature babies room),  vyumba kwa ajili ya ofisi za madaktari na manesi, chumba cha kuzalia (Labour room) na pia kuna chumba cha kufulia nguo za wagonjwa.walio," alisema Dr. Lutambi.

Uzinduzi wa wodi huo umehudhuriwa na Naibu waziri wa maliasili na utalii, Mahamood Mgimwa, ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Mufindi Kaskazini.

WANAWAKE MILIONI MOJA WAANDAMANA NIGERIA KUPINGA KUSHINDWA KWA SERIKALI KUWAOKOA MAMIA YA WASICHANA WA SHULE



Shirika la kutetea wanawake nchini Nigeria limeitisha maandamano ya wanawake milioni moja katika mji mkuu , Abuja kupinga kushindwa kwa serikali kuwaokoa mamia ya wasichana wa shule waliotekwa nyara na Boko Haram.
Wazazi waliojawa ghadhabu wameishutumu serikali ya Nigeria kwa kushindwa kuwaokoa wasichana hao waliotekwa nyara kutoka shule moja ya upili katika mji wa Chibok lililopo jimbo la Borno tarehe 14 mwezi huu.
Shambulizi hilo linaloshukiwa kufanywa na waasi wa Boko Haram ni miongoni mwa mabaya zaidi kuwahi kuripotiwa nchini humo katika kipindi cha hivi karibuni yanayolenga asasi za elimu.
Ghadhabu nchini humo zimeongezeka zaidi kutokana na jeshi la nchi hiyo kushindwa kuwapata wasichana hao zaidi ya wiki mbili sasa.
Maafisa wa jimbo la Borno wamesema kiasi cha wanafunzi 129 walitekwa nyara na wapiganaji wa Boko Haram waliowalizimisha kuingia katika msafara wa malori na kutorokea msituni na 52 kati ya wasichana hao waliweza kujiokoa.

BAADA YA MIAKA 40 ATLETICO MADRID YATINGA FAINALI UEFA YAICHAKAZA CHELSEA 3 - 1



Klabu inayoongoza ligi ya Uhispania almaarufu kama La Liga ATletico Madrid usiku huu imefanikiwa kuingia fainali ya Klabu bingwa ya Ulaya UEFA baada ya kuicharaza Chelsea ya Uingereza pale nyumbani kwake darajani mbele ya mashabiki wake 3 - 1, ambapo sasa Atletico Madrid atakutana na Real  Madrid katika fainali timu zote zikiwa ni kutoka nchini Hispania. Chelsea walikuwa wa kwanza kupata goli kupitia mchezaji wake Torres katika dakika ya 36 na dakika 44 kabla ya kupulizwa filimbi ya mapumziko Atletico Madrid kupitia Adrian Lopez walisawazisha. Katika dakika ya 60 Diego Costa aliipatia Atletico goli la pili kwa mkwaju wa penati iliyosababishwa na Etoo baada ya kumsukuma kwa nyuma mchezaji wa Atletico Madrid na goli lililokata matumaini ya Chelsea ni goli lililofungwa na Arda Turan katika dakika ya 72. Katika mechi ya awali timu hizo zilitoka 0 – 0. Atletico Madrid kwa mara ya kwanza inafika fainali ya Klabu bingwa ya Ulaya baada ya miaka 40.

LUGHA YA KIBAGUZI YAMPONZA MMILIKI WA TIMU YA KIKAPU YA L.A. CLIPPERS

Tarehe 29 April, 2014, Sterling alifungiwa maisha na NBA kutojihusisha na masuala ya mpira wa kikapu. Pia alipewa adhabu ya kulipa faini ya $2.5 milioni na kuuza hisa zake zote za Los Angeles Clippers baada ya maongezi yake ya kibaguzi dhidi ya watu weusi yaliyorekodiwa kuwekwa hadharani.
Sterling alikuwa mmiliki wa A.L. Clippers kuanzia mwaka 1981 baada ya kuinunua kwa kitita cha $12.5 milioni, na hadi kufikia mwaka 2014, A.L. Clippers ilikuwa na thamani ya $575 milioni kwa mujibu wa gazeti la Forbes. Sterling alikuwa ni mmiliki wa timu ambayo inashiriki ligi ya NBA wa muda mrefu.

MIKATABA YA KIMATAIFA YAPINGA VIKALI UTUMIKISHWAJI KWA WASICHANA WALIO CHINI YA MIAKA 18



Shirika la Kazi Ulimwenguni ILO limebainisha kwamba kazi za ndani zinazofanywa na wasichana walio chini ya miaka 18 katika mazingira ya kitumwa, hatari au kinyonyaji ni aina ya utumikishwaji wa watoto unaotakiwa kutokomezwa kama ilivyoainishwa kwenye mikataba ya kimataifa.
Mikataba hiyo inapinga utumikishwaji huo kufuatia kukithiri kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia, udhalilishaji, kunyimwa chakula, kubakwa na kulipwa mishahara kiduchu huku wahusika wakishindwa kuripoti kwa wazazi au katika vyombo vya usalama.
Umaskini umekuwa ukichangia kwa kiasi kikubwa wazazi kuwaruhusu watoto wao kwenda kutumikishwa majumbani, hata hivyo sababu ya ukosefu wa elimu inawagusa baadhi ya wazazi nchini
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu LHRC ni moja ya taasisi zilizo mstari wa mbele katika kutetea haki za wasichana wanaofanyiwa ukatili wa kijinsia na waajiri wao.
 Wachungaji ni moja ya kundi linalowajibika kwa kiasi kikubwa kuhakikisha jamii haiendi kinyume cha mila, desturi na maadili ya Kitanzania, Mchungaji FESTUS SAMBWE wa Kanisa la Tanzania Assembles Of  God Kihonda Morogoro ametoa wito kwa wazazi kujiepusha na tabia kuwaruhusu watoto kujiingiza kwenye ajira zisizo rasmi.
Tayari tumeshuhudia athari, madhira na changamoto wanazokumbana nazo wafanyakazi wa ndani ambao wazazi wamewafanya kama miradi katika kuwakomboa kwenye umaskini.

JAMII IMEHIMIZWA KUWA KARIBU NA POLISI



Jamii imehimizwa  kuwa karibu na jeshi la polisi katika kuhakikisha hakuna wahalifu wanaojipenyeza katika mitaa na kusababisha uharibifu wa amani pamoja na mali  za wananchi.
Akiongea katika  uwekaji wa jiwe la msingi la kituo kikubwa cha polisi kinachotarajiwa kujengwa katika kata ya Segerea jijini Dar es salaam ,Naibu mkuu wa jeshi la polisi nchini ABRAHMANI KANIKI,  amesema  kuwepo kwa kutuo hicho kutasaidia sana kuondoa wasiwasi wa raia na mali zao.
Wakiongea katika uzinduzi huo  Mbunge wa jimbo hilo  ambae pia ni Naibu waziri wa kazi na ajira MAKONGORO MAHANGA na diwani wa kata hiyo AZURI MWAMBIJI wamesema katika kutumikia jamii wameweka tofauti zao pembeni ili kuhakikisha wananchi wa eneo hilo wanapata kituo kikubwa cha polisi kwa ajili ya kuimarisha usalama. 
Katika  uzinduzi huo uongozi wa Bank ya posta TANZANIA umekabidhi hundi ya shilingi million kumi kama mchango wao kwa ujenzi wa kituo hicho.

MAMIA YA WAKAZI WA SINGIDA WAJITOKEZA KUAGA MIILI YA ASKARI POLISI WANNE WALIOGONGWA NA GARI



Mamia ya wakazi wa mji wa Singida wamejitokeza kuaga miili ya askari Polisi wanne waliokufa kwa kugongwa na basi la kampuni ya Sumry lililokua likitokea kigoma kuelekea Dar es salaam.
Akizungumza wakati wa ibada ya kuombea marehemu hao iliyofanyika katika viwanja vya Polisi line, Paroko YONAS MLEWA wa kanisa kuu Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, amewataka askari polisi wasikatishwe tamaa na matatizo wanayopata kazini, ikiwemo vifo.
 Aidha Paroko huyo ameikumbusha Serikali kuboresha mazingira ya kazi kwa askari wanaojitoa kwa nguvu zote katika kuwatumikia Watanzania
 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida GEOFREY KAMWELA amesema askari waliopoteza maisha bado vijana ambao wangetumikia taifa kwa muda mrefu, huku MEJA CHRISTINA MICHAEL akiishukuru jamii mkoani Singida kwa kuonyesha moyo wa upendo katika msiba huo…
Kufuatia ajali hiyo Rais JAKAYA KIKWETE amemtumia salam za rambirambi mkuu wa mkoa wa singida Dr. PARSEKO KONE kufuatia vifo vya watu 19 wakiwemo askari polisi hao wanne na viongozi watatu wa kijiji.
Rais kikwete amemuomba mkuu wa mkoa wa singida  kumfikishia salam zake za rambi rambi na pole kwa watu waliopotelewa na ndugu na jamaa zao na anawaombea majeruhi waweze kupona haraka. 

Ajali hiyo imetokea wakati watu wakiwa wamekusanyika kando ya barabara kushuhudia askari hao wakipakia kwenye gari mwili wa mwendesha baiskeli GERALD ZEFANIA aliyekufa kwa kugongwa na lori, ndipo basi hilo lilipowapitia na kukatiza maisha yao.