Mamia ya wakazi wa mji wa Singida wamejitokeza kuaga
miili ya askari Polisi wanne waliokufa kwa kugongwa na basi la kampuni ya Sumry
lililokua likitokea kigoma kuelekea Dar es salaam.
Akizungumza wakati wa ibada ya kuombea marehemu hao
iliyofanyika katika viwanja vya Polisi line, Paroko YONAS MLEWA wa kanisa kuu
Parokia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, amewataka askari polisi wasikatishwe tamaa
na matatizo wanayopata kazini, ikiwemo vifo.
Aidha Paroko huyo ameikumbusha
Serikali kuboresha mazingira ya kazi kwa askari wanaojitoa kwa nguvu zote
katika kuwatumikia Watanzania
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida
GEOFREY KAMWELA amesema askari waliopoteza maisha bado vijana ambao
wangetumikia taifa kwa muda mrefu, huku MEJA CHRISTINA MICHAEL akiishukuru
jamii mkoani Singida kwa kuonyesha moyo wa upendo katika msiba huo…
Kufuatia ajali hiyo Rais JAKAYA KIKWETE amemtumia
salam za rambirambi mkuu wa mkoa wa singida Dr. PARSEKO KONE kufuatia vifo vya
watu 19 wakiwemo askari polisi hao wanne na viongozi watatu wa kijiji.
Rais kikwete amemuomba mkuu wa mkoa wa singida
kumfikishia salam zake za rambi rambi na pole kwa watu waliopotelewa na
ndugu na jamaa zao na anawaombea majeruhi waweze kupona haraka.
Ajali hiyo
imetokea wakati watu wakiwa wamekusanyika kando ya barabara kushuhudia askari
hao wakipakia kwenye gari mwili wa mwendesha baiskeli GERALD ZEFANIA aliyekufa
kwa kugongwa na lori, ndipo basi hilo lilipowapitia na kukatiza maisha yao.
No comments:
Post a Comment