(Zahanati ya Ibumu)
Diwania wa kata ya Ibumu, Hemed Mbena |
BAADHI ya wanawake wenye maambukizi ya
virusi vya Ukimwi (VVU) wa kijiji cha Ibumu wilayani Kilolo mkoani Iringa wameelezwa
kuwaambukiza kwa makusudi vijana wenye tamaa ya kupata fedha kutoka kwao.
Taarifa za wanawake hao ambao hata hivyo
hawakutajwa majina yao katika mtandao huu zimeelezwa kuripotiwa kwa uongozi wa
serikali ya kata ya Ibumu kilipo kijiji hicho.
Muuguzi wa Zahanati ya Kijiji hicho,
Spesioza Fivao alisema pamoja na kushitakiwa, wanawake hao ambao baadhi yao
wanapata huduma ya dawa za kupunguza makali ya VVU (ARV) katika kituo chao
wameendelea kuwachangamkia vijana hao.
Fivao alisema; “hili sio jambo la siri,
unajua kwa kijiji kidogo kama hiki tunajuana, na baadhi ya watu wenye
maambukizi hayo wanajulikana, pamoja na hayo yote wanachangamkiwa na vijana hao
kwasababu wanadaiwa kutoa pesa zinazowawezesha vijana hao kujikimu kimaisha.”
Diwani wa kata hiyo, Hemed Mbena
amethibitisha kuwepo kwa changamoto hiyo inayozidisha kasi ya maambukizi ya VVU
katika kata yake.
Mbena alisema baadhi ya vijana hao
wametumbukia katika tatizo hilo kwasababu tu ya kununuliwa pombe na wanawake na
wanaume wenye maambukizi hayo.
Alisema wengine wanaishi kama mume na mke
pamoja na kwamba wakati wakikutana kwa mara ya kwanza mmoja wapo alikuwa hana
maambukizi hayo.
Mwaka 2011, Wizara ya Katiba na Sheria
iliahidi kuwachukulia hatua kali watu watakaobainika kueneza kwa makusudi virusi vya Ukimwi kwa watu
wengine.
Sheria ya kudhibiti na kupambana na
virusi vya Ukimwi na Ukimwi, kifungu cha 176 cha kanuni ya adhabu (penal code),
sura ya 16 kinaeleza wazi kuwa ni kosa la jinai kwa mtu yeyote ambaye bila
uhalali au kwa uzembe, anafanya kitendo chochote ambacho anajua kuwa
kitasababisha kuenea kwa ugonjwa hatari wa binadamu.
Anayepatikana na hatia kwa mujibu wa
sheria hiyo anaweza kufungwa kifungo cha miaka miwili, kutozwa faini au vyote
viwili.
Wakati huo huo serikali imeendelea kutoa wito
kwa Watanzania kutoa taarifa za watu wenye kueneza magonjwa ya kuambukiza kwa makusudi
wakati wakijua wazi kuwa ni kosa la jinai.
Nchini Kenya mtu anayekutwa na hatia hiyo
anaweza kuhukumiwa hadi miaka 15 jela.
No comments:
Post a Comment