Thursday, May 29, 2014

Mmiliki Wa Manchester United Afariki Dunia

Malcom Glazer aliyehinda tenda ya utata ya kuichukua Manchester United mwaka 2005 amefariki dunia jana akiwa na umri wa miaka 85. Mfanyabiashara huyo wa Marekani atakumbukwa kama bilionea wa Florida aliyeichukua kuimiliki United miaka tisa iliyopita na kuwekeza zaidi ya pauni milioni 500, Glazer mkubwa amekuwa mgonjwa kwa muda sasa na kuwaachia shughuli za uendeshaji wa United watoto wake wa kiume, Joel na Avran.
Msemaji wa Manchester United: “fikra za kila mmoja katika United zipo kwa familia usiku” Familia ya Glazer bado wanamiliki Tampa Bay Buccaneers, timu ya mpira wa miguu ya Marekani waliyoinunua mwaka 1995.

Al Sisi ashinda kwa kishindo uchaguzi wa rais Misri

Kiongozi wa zamani wa jeshi Abdel Fattah al Sisi ameibuka na ushindi mkubwa katika uchaguzi wa rais nchini Misri. Amejikingia zaidi ya asili mia 90 ya kura lakini walioteremka vituoni inasemekana ni asilimia 44 tu.

Kiongozi huyo zamani wa jeshi, kwa mujibu wa duru za sheria amepata asilimia 93 nukta 3 ya kura wakati shughuli za kuhesabu kura zikiwa tayari zimekamilika. Mgombea Hamdine Sabahi, mpinzani pekee katika uchaguzi huo amepata asilimia 3 nukta 8 ya kura, huku asilimia 3 nukta 7 ya kuwa ikiwa ni kura zilizoharibika.

Lakini idadi ya walioshiriki kupiga kura ikadiriwa asilimia 44 nukta 4, kwa mujibu wa duru hizo na hivyo kuweka shaka kwenye uhalali wa Al- Sisi, muasisi wa mapinduzi yaliyomuondowa madarakani Julai mwaka jana rais aliyechaguliwa kidemokrasia Mohamed Morsi.
Yalipoanza kutangazwa matokeo ya uchaguzi, wafuasi wa Al Sisi walizunguka barabara za Cairo na kupeperusha bendera wakisheherekea ushindi wa mgombea wao, huku honi za gari zikisikia katika mji mkuu.

Usiku kucha wafuasi hao wa Jemedari mstaafu Sisi walijumuika wakiimba na kucheza kwenye eneo maarufu la Tahrir lililoshuhudia maandamano makubwa yaliyompinduwa aliyekuwa rais wa Msri, Hosni Mubarak Novemba 2011, baada ya kuiongoza Misri kwa zaidi ya miaka 30.

Rais Wa Nigeria Goodluck Jonathan Aagiza Operesheni Kali

Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan ameagiza kufanywa oparesheni kali zaidi ili kudhibiti alichokiita mauaji ya kiholela yanayofanywa na magaidi.
Katika hotuba kwa taifa kuadhimisha siku ya demokrasia, rais Jonathan alitaja utekaji nyara wa zaidi ya wasichana mia mbili wa shule na kundi la Boko Harama kuwa unyama usiokubalika kamwe.
Waandishi hata hivyo wanasema kuwa haijulikani rais Jonathan anazungumzia kuchukua hatua zipi au ni oparesheni gani itafanywa kwa sababu tayari eneo hilo la Kaskazini mashariki mwa Nigeria tayari limewekwa chini ya hali ya hatari.
Rais Jonathan pia ameahidi kufanya mashauriano na upatanishi na watu watakaoweka silaha chini na kukoma kujihusisha na ugaidi.

Kiongozi wa kundi la Boko Haram Abubakar Shekahu
Alipongeza jamii ya kimataifa kwa kuisaidia Nigeria kukabiliana na tatizo la ugaidi na usalama kwa jumla.
Rais Jonathan ameahidi kushughulikia swala la umasikini ambalo limechochea harakati kama za Boko Haram, lakini akasisitiza hilo litafanyika tu ikiwa ugaidi unaotendwa na Boko Haram utakomeshwa.

Benki ya dunia inasema kuwa zaidi ya watu milioni miamoja na kumi na tatu wanaishi kwa umaskini katika taifa hilo linalozalisha kiwango kikubwa zaidi cha mafuta Afrika.
Rais Goodluck, ametoa fursa kwa Boko Haram ikiwa wanataka kufanya mazungumzo na serikali kama njia ya kusuluhisha matatizo yao.

Maelfu ya watu wameuawa katika miaka mitano ya harakati za kundi hilo.Mwaka huu pekee watu 2,000 wameuawa huku zaidi ya wengine 750,000 wakiachwa bila makao.

Wasichana Wawili Wabakwa Kisha Kunyongwa Nchini India

Wasichana wawili wa kihindi waliopatikana wakiwa wananing'inia kwenye mti katika jimbo la Uttar Pradesh, walikuwa wamebakwa kisha wakanyongwa.
Polisi wanasema kuwa mwanamume mmoja amekamatwa kuhusiana na mauaji hayo huku polisi watatu wakiachishwa kazi kwa kutosajili kesi hiyo iliporipotiwa kuwa wasichana hao walikuwa wametoweka, kabla ya kupatikana wakiwa wameuawa.
Wasichana hao walipatikana katika wilaya ya Badaun na wanadhaniwa kuwa na umri mdogo kuanzia 13 hadi 15
Ubaguzi dhidi ya wanawake umekita mizizi katika jamii nyingi nchini India.
Visa vya dhuluma za kingono vimeendelea kukithiri nchini India tangu mwaka 2012 ambapo msichana mmoja alibakwa na genge la vijana hadi kufa
Serikali ililazimika kuweka sheria kali kwa wanaopatikana na hatia ya kutenda vitendo vya dhuluma za kingono baada ya maandamano kufanyika kote nchini kufuatia shambulizi hilo.
Polisi mmoja alisema kuwa wasichana hao walikuwa na uhusiano wa kifamilia na walipatwa wakiwa wananing'inia kwenye mti kijiji cha Badaun mnamo siku ya Jumatano.
Alisema kuwa polisi wanawasaka wanmaume wawili waliowabaka wasichana hao na kisha kuwanyonga.
Wasichana hao walichomwa kuambatana na tamaduni za maziko ya kihindi Jumatano.
Polisi wanasema wanachunguza ambavyo wasichana hao walipotea, kubakwa na kisha kuwekwa kwenye mti.
(By BBC).

Uchina Imeanza Kulegeza Sheria Zake Za Mpango Wa Uzazi

Uchina imeanza kulegeza sheria zake za mpango wa uzazi, na sasa inapiga kampeni ya kuongeza angalau watoto millioni mbili zaidi wanaozaliwa kila mwaka.
Serikali itaongeza wakunga na wahudumu sambamba na kupanua nafasi hospitalini na kuongezwa idadi ya vitanda na vifaa vinginevyo.
Kwa muda mrefu Uchina imeendeleza sera kali ya mpango wa uzazi ya kulazimu familia kuwa na mtoto mmoja tu, huku wanaokiuka wakichukuliwa hatua kali jambo linaloshutumiwa kimataifa.
Lakini mwaka jana serikali ilianza kulegeza kamba kwa kusema iwapo mmoja wa wazazi amekuwa mtoto wa pekee katika familia, basi anaweza kuzaa mtoto wa pili.
Japo hatua za awali zilichukuliwa kukabiliana na idadi kubwa ya watu nchini humo, sasa kumetokea mapungufu ambayo yanahitaji kusawazishwa.
Nao Wapanga sera wamependekeza juhudi hizo za kuongeza idadi ya watoto, zichukuliwe sasa la sivyo Uchina itajikuta na upungufu mkubwa wa nguvu kazi za vijana, huku idadi ya wazee na wanaostaafu ikiwa kubwa kiasi cha kuzorotesha uchumi wa taifa hilo kubwa duniani.

Watendaji Wa Halmashauri Ya Wilaya Ya Mbulu Wameagizwa Kuhakikisha Wanaweka Mipango Mizuri Ya Matumizi Bora Ya Ardhi

Watendaji wa Halmashauri ya wilaya ya MBULU mkoani MANYARA wameagizwa kuhakikisha wanaweka mipango mizuri ya matumizi bora ya Ardhi, ili kuepusha migogoro baina ya WAFUGAJI na WAKULIMA inayosababisha wakati mwingine umwagikaji wa Damu.
Katibu mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM, ABDULRAHMAN KINANA ametoa kauli hiyo, baada ya kutembelea eneo la bonde la YAEDA wilayani humo, na kupata malalamiko ya wananchi hao kuhusiana na mgogoro wa Ardhi kati ya WAFUGAJI, WAKULIMA na WAWEKEZAJI, wanaodaiwa kudhulumu ardhi ya wanyonge katika eneo hilo.
Wakitoa malalamiko hayo kwa katibu mkuu  wa CCM,  wananchi hao wamedai kuwepo kwa kikundi cha watu kinachotumia mabavu na fedha,   kuwaondoa  kutoka katika maeneo yao ya Asili kwa lengo la kutwaa ardhi ya wananchi hao ambao wengi wao ni masikini.
Kufuatia malalamiko hayo katibu mkuu wa CCM amekiri kuwa, migogoro mingi ya Ardhi inayochukua sura mpya kila siku na umwagikaji wa damu kwa wasiokuwa na hatia, inachangiwa zaidi na Watendaji wa Serikali kushindwa kutoa elimu kuhusu matumizi bora ya Ardhi kwa Jamii za WAFUGAJI na WAKULIMA, huku mkuu wa wilaya ya Mbulu ANATOLY CHOYA akielezea mikakati ya Serikali katika kukabiliana na tatizo hilo. 
Mkoa wa MANYARA ni miongoni mwa maeneo yenye migogoro mingi ya Ardhi, inayochangia umasikini kwa watu wake kwa kuwa wanatumia muda mwingi katika kushughulikia migogoro hiyo, kuliko kufanya kazi za Maendeleo.

Baada Ya LHRC Kuzindua Ripoti Ya Taarifa Kuhusu Madhara Yanayotokana Na Uchimbaji Baadhi Ya Wananchi Waeleza Haina Haja Serikali Kusitisha Uchimbaji

Siku moja baada ya kituo cha sheria na haki za binaadamu LHRC,  kuzindua  ripoti ya taarifa kuhusu madhara kwa afya na mazingira ya madini ya urani,  baadhi ya wananchi wamesema  hakuna haja ya Serikali kusitisha uchimbaji wa madini hayo, badala yake ziwekwe njia madhubuti za kudhibiti madhara.  
Wakazi hao VEDASTO MKAKA, MAIMUNA IDDY, NA ADNANI MITEMA wamesema,  uzoefu unaonyesha kuwa sio Tanzania  pekee yenye madini kama hayo, hivyo kuacha kuyachimba kwa kuhofia madhara sio jambo la msingi, na wametumia fursa hiyo kuwaomba wanaharakati hao kushirikiana na serikali, kutafuta ufumbuzi wa hali hiyo. 
 
Aidha akizungumza katika uzinduzi huo, mkurugenzi wa  kituo cha sheria na haki za binaadam  Bi. HELEN KIJO BISIMBA amesema, uzoefu  wa kitaalamu kutoka katika nchi ambazo madini hayo yanazalishwa unaonesha kuwa, zoezi la uchimbaji wa madini hayo linahitaji  kiwango kikubwa cha maji, huku athari kwa jamii  kuhusu magonjwa ya ngozi na kansa ikihofiwa kuwa kwa kiasi kikubwa.
Naye makamu mwenyekiti wa tume ya haki za binadamu na utawala bora  MAHAFUDHA HAMID amesema,  uzoefu kutoka katika machimbo mengi ya madini hapa nchini unaonesha kuwepo kwa baadhi ya vitendo vya uvunjifu wa haki za binaadamu hivyo vyema sera ya madini ya urani ikawekwa wazi kutokana  na hatari iliyomo katika madini hayo, ili kuepusha vitendo hivyo kutojitokeza.
Nayo baadhi ya Maeneo yaliyofanyiwa utafiti na kubainika kuwa na madini ya urani ni  Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma.
Miongoni mwa maeneo hapa nchini ambayo madini ya urani yanategemewa kupatikana ni pamoja na NAMTUMBO, MANYONI na BAHI.

Imeelezwa Kuwa Maambukizi Ya Virusi Vya Ukimwi Yamepungua Nchini

Imeelezwa kuwa maambukizi ya virusi vya UKIMWI nchini yamepungua kutoka asilimia 5.7 mwaka 2008, na kufikia asilimia 5.1 kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa Machi  2013, huku Pemba ikiwa na maambukizi madogo ambayo ni kati ya asilimia 0.1 na 0.4.
Waziri wa Nchi, Sera, Uratibu na Bunge WILLIAM LUKUVI ameliambia Bunge, wakati akijibu swali la mbunge wa Wete MBAROUK SALIM ALI, kuwa mikoa mingi yenye maambukizi makubwa haifanyi tohara kwa wanaume ukiwemo mkoa wa Njombe wenye asilimia 14.8, Iringa asilimia 9.1, Mbeya asilimia 9, Shinyanga asilimia 7.4, Ruvuma asilimia 7, Dar es Salaam asilimia 6.9, Katavi asilimia 5.9 na mkoa wa Pwani asilimia 5.9.

Serikali Yatakiwa Kufanyia Kazi Marekebisho Sheria Ya Uchaguzi Wa Serikali Za Mitaa

Serikali imetakiwa kukamilisha taratibu zote muhimu, ikiwemo kuifanyia marekebisho sheria ya uchaguzi wa Serikali za mitaa, ili kuepusha dosari zilizojitokeza katika uchaguzi uliopita.
Rai hiyo imetolewa na kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni FREEMAN MBOWE, wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu MIZENGO PINDA ambaye amesema, hatua iliyoanza ni maandalizi ya bajeti huku taratibu zikifanyika, kuangalia maeneo yote muhimu yakiwemo yanayolalamikiwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Mbunge wa Kilwa MURTAZA MANGUNGU amemtaka Waziri Mkuu kuingilia kati, mkanganyiko wa uongozi katika jiji la Dar es Salaam kuhusu suala la uchafu uliokithiri jijini humo, kunakotokana na Halmashauri kuacha baadhi ya majukumu kwa kisingizio kuwa ni jukumu la jiji, jambo ambalo Waziri Mkuu MIZENGO PINDA ameshauri lianzie katika ngazi ya chini.

Sunday, May 25, 2014

BALE ATIMIZA NDOTO YA REAL MADRID KUCHUKUA KLABU BINGWA ULAYA KWA MARA YA 10

BALE
Real Madrid wamekuwa mabingwa wa Uefa 2014 baada ya kuilaza Atletico Madrid kwa jumla ya magoli ya 4 – 1 katika mchezo uliokuwa na kasi na wa nguvu na akili ulipigwa jijini Lisbon Ureno , Atletico ndio waliokuwa wakwanza kuliona lango la Real Madrid kwa goli lililofungwa na Godin katika dakika 36. 
Goli hilo lilidumu hadi dakika ya 90 pale Ramos alipowainua mashabiki wa Real Madrid kwa kusawazisha na kupelekea kuongezwa dakika nyingine 30. Katika dakika 15 za mwanzo dakika ya 110 Bale alifunga goli la pili, katika dakika 15 za kipindi cha pili wa muda wa nyongeza dakika ya 18 Marcelo akaipatia Real Madrid bao na kuvunja kabia matumaini kwa timu ya Atletico Madrid. 
Ronaldo akafungwa kwa mkwaju wa penati dakika ya 120 na kuifanya Real Madrid kuwa mabingwa wa Uefa 2014 ikiwa ni mara ya 10 na ikiongoza kulichukua kombe hilo mara nyingi kuliko timu yeyote ya barani Ulaya. Ronaldo anaongoza kwa kufunga magoli mengi msimu huu kwa idadi ya magoli 17, akifuatiwa na Ibrahimovic wa PSG ana magoli 10, Diego Costa wa Atletico Madrid na idadi ya magoli 8, akifuatiwa na Messi nae anamagoli 8 wakiwa wamelingana, Aguero wa Man City anayo magoli 6.
 

Friday, May 23, 2014

DAR ES SALAAM INAONGOZA KWA WATU WENGI KWA MUJIBU WA SENSA YA WATU NA MAKAZI YA MWAKA 2012

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 nchi ya Tanzania ina zaidi ya watu Milioni 44, ambapo Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kuliko mikoa yote nchini, wenyewe ukiwa na watu wanaofikia milioni 4.3.
Licha ya takwimu hizo kuonesha ongezeko hilo la watu kutoka Milioni 36 mwaka 2002 hadi kufikia Milioni 44.5, tafiti zinaonesha kuwepo kwa watoto wengi wanaoishi kwenye mazingira magumu, kwenye Wilaya 108 nchini mwaka 2012/  2013 ambapo Wavulana ni 474, 424 sawa na asilimia 53 huku Wasichana  wakiwa 420, 424 sawa na asilimia 47.
Kutokana na changamoto hiyo imebainika kuwa kati ya watoto hao, zaidi ya 70 miongoni mwao wanaishi katika kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi Ubungo na kukutana na kiongozi wao anayefahamika kwa jina maarufu RAMA FUNDI.
Sheria ya Haki za Mtoto iliyotafsiriwa mwaka 2009 inabainisha masuala mbalimbali ikiwemo mtoto kutotengwa, kujua jina au utaifa wake, kuishi na wazazi ama walezi ikiwemo wajibu wa kumtunza mtoto, kama ilivyo sheria ni msumeno,  je watoto hao wanazijua haki zao ili kuweza kukabiliana na matatizo wanayokumbana nayo? 
Dawati la Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu LHRC lililo chini ya Ofisa Mradi wake Wakili NAEMI SILAYO lina wajibu wa kuhakikisha haki za watoto hazipindishwi, kama sheria ya watoto ya mwaka 2009 inavyobainisha.
Serikali kupitia Maafisa Watendaji nao kwa nafasi zao wanawajibika kuhakikisha watoto katika maeneo yao wanapatiwa haki zao ikiwemo ya kucheza na kufurahia maisha, je nao wamechukua juhudi zozote katika kuwasaidia watoto hao.
Mke wa Rais Mama SALMA KIKWETE amewahi kusema, MTOTO WA MWENZIO NI WAKO UMLINDE, je umeshawahi kuchukua juhudi zozote za kuwalinda watoto wanaonyanyaswa katika jamii yako, kama bado chukua hatua.

SERIKALI IMETAKIWA KUWEKA MIPANGO YA MATUMIZI BORA YA ARDHI

Serikali imetakiwa kuweka mipango ya matumizi bora ya ardhi kwa kutenga maeneo ya wakulima na wafugaji ili kuepusha migogoro ya mara kwa mara ya wakulima na wafugaji, ambayo imekuwa ikisababisha vifo vya wananchi na mifugo katika maeneo mbalimbali nchini.
Rai hiyo imetolewa na Kamati ya Bunge ya kilimo, mifugo na maji kupitia kwa mwakilishi wake AMINA MAKILAGI na Kambi Rasmi ya upinzani bungeni kupitia kwa Waziri Kivuli wa Mifugo na Uvuvi ROSEMARY KAMILI wakati wakitoa maoni kwa makadirio ya mapato na matumizi ya wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2014/2015.
Pamoja na rai, suala na kuiwezesha sekta ya mifugo kuchangia pato la Taifa limezungumziwa, huku Kambi rasmi ya upinzani bungeni ikitaka kuwasilishwa bungeni kwa taarifa ya uchunguzi ya kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kuhusu migogoro ya wakulima, wafugaji na hifadhi, huku wakitaka kufutwa kwa kodi ya mifugo.
Awali akiwasilisha hotuba ya makadirio ya bajeti ya Wizara yake kwa mwaka 2014/2015 suala la oparesheni tokomeza, waziri wa Mifugo na Uvuvi Dk. TITUS KAMANI ameahidi kutenga maeneo maalum kwa ajili ya wafugaji ikiwa ni sehemu ya kupunguza migogoro baina ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi huku akibainisha kuwepo kwa ongezeko la uzalishaji wa nyama.
Tanzania ina jumla ya Ngombe milioni 22.8, Mbuzi milioni 15.6, Kondoo milioni 7, Nguruwe milioni 2.01, Kuku wa Asili milioni 35.5 na Kuku wa kisasa milioni 24.5.

KUTOKANA NA MATUKIO YA MILIPUKO YA MABOMU KATIKA BAADHI YA NCHI ZA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI WANANCHI WATAKIWA KUSHIRIKI KIKAMILIFU KATIKA KUPIGA VITA VITENDO HIVYO

Kufuatia kuwepo kwa mfululizo wa matukio ya milipuko ya mabomu katika baadhi ya nchi za jumuiya ya Afrika mashariki hasa katika kipindi cha hivi karibuni, wananchi wa ukanda huo wametakiwa kushiriki kikamilifu kupiga vita ugaidi badala ya kuziachia serikali za nchi husika pekee.
Rai hiyo imetolewa na mwenyekiti wa kamati ya mahusiano na utatuzi wa migogoro katika ukanda wa Afrika mashariki Abubakari Zein katika mkutano unaojadili hali ya amani na utatuzi wa migogoro, ambayo katika kipindi hiki matukio ya kigaidi yameelezwa kuongezeka.
Nchi ya Kenya imeshuhudia matukio kadhaa ya milipuko inayodaiwa kuhusishwa na ugaidi.
Washiriki kutoka pande mbali mbali za Afrika mashariki wamehudhuria mkutano huo akiwemo Benard Murunya kutoka Tanzania ambae anabainisha kuwa mkutano huo ni muhimu kutokana na matukio yanayoendelea katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki.
Mkutano huo umewakutanisha wabunge wa bunge la Afrika  mashariki  lengo likiwa ni kujadili hali ya usalama na matukio ya kigaidi yanayoendelea kushamiri ambapo mwaka jana mlipuko mkubwa katika jengo la biashara la WESTGET nchini Kenya uliuwa watu wapatao 67.

KATANGA AHUKUMIWA MIAKA 12 JELA

Mahakana ya Kimataifa ya Uhalifu ya mjini The Hague Uholanzi imemuhukumu mbambe wa kivita kutoka Congo, Germain Katanga, miaka 12 gerezani baada ya kukutwa na hatia ya kuwapa silaha kundi la waasi 2003 na kufanya mauwaji.
"Mahakama imemuhukumu Germain Katanga kifungo cha miaka 12 gerezani," alisema Jaji Mkuu Bruno Cotte mbele ya mahakama ya The Hague ikiwa ni hukumu yake ya pili tangu kufunguliwa kwake mwaka 2003. Jaji huyo amesema kile kipindi cha miaka saba ambacho mtuhumiwa amekutimia akiwa kizuizini kitapunguzwa katika miaka ya kifungo chake.

Mwezi Machi mwaka huu, Katanga mwenye umri wa miaka 36, alikutwa na hatia ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamu, yakiwemo mauwaji na uporaji kutokana na jukumu lake katika harakati za kuvamia kijiji cha Bogoro katika eneo tete la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tarehe 24 Februari 2003.

Wakati ikitangazwa hukumu hiyo, Katanga ambaye anajulikana kwa jina la utani la Simba, hakuonesha mtikisiko wowote mahakamani hapo. Inaelezwa kuwa matukio hayo ya uhalifu yalifanyika wakati akiwa na umri wa miaka 24.
Jaji aligundua kuwa alilipa silaha kundi la wapiganaji la Patriotic Resistance Forces la mjini Ituri (FRPI) ambalo liliuwa idadi kubwa ya watu, ikikadiriwa kuzidi 200. Jaji Cotte ameiambia mahakama ya ICC kwamba makovu ya mapigano ya Februari 24, 2003 yameendelea kuonekana mpaka leo hii. Amesema kutumika kwa mapanga katika mashambulizia hayo ilikuwa vitendo vya kikatali sana na kwamba kumesababisha maumivu yaliyokithiri.

Hata hivyo, awali mahaka ya uhalifu wa kivita ICC ilimfutia mashitaka Katanga ya ubakaji, utumwa wa kingongo, na kutumia watoto wenye umri mdogo jeshini. Baada ya kutolewa hukumu hiyo wanasheria kutoka kwa upande wa Katanga watakuwa na siku 30 ya kukataa rufaa kufuatia hatua hiyo. Hata hivyo uhamuzi rufaa hiyo bado haujatolewa.
Hukumu hio ni ya pili kutolewa tangu kufunguliwa milango ya mahakama hiyo mwaka 2003, nyingine ilikuwa ya mbambe wa kivita ambae kwa wakati fulani alikuwa hasimu wake Thomas Lubanga ambae mwaka Julai 2012 alihukumiwa miaka 14 gerezani.

VATICAN INAPUUZA HAKI ZA WATOTO - UMOJA WA MATAIFA

Kamati ya Umoja wa Mataifa dhidi mateso imelaumu vikali kanisa Catholiki kwa kutoshughulikia ipasavyo suala la unyanyasaji wa ngono ndani ya kanisa hilo.
Katika ripoti iliyochapishwa hivi karibuni na Umoja huo mjini Geneva , Kamati hiyo imeushutumu utawala wa Vatican kwa kuwahamisha watawa kutoka parokia moja hadi nyingine kuwaepusha kushtakiwa, na kupuuza haki za waathiriwa za kupokea fidia .

Utawala wa Vatican uliithinisha mkataba dhidi ya unyanyasaji , ukatili na matendo yaliyo kinyume na utuUchunguzi uliofanywa na kamati ya Umoja wa Mataifa dhidi ya Vatcan ni sehemu ya uchunguzi wa mara kwa mara wa kamati hiyo dhidi ya nchi wanachama ili kuhakikisha mikataba inatekelezwa.
Kamati hiyo ya Umoja wa Mataifa ina hofu kuwa wakati utawala wa Vatcan umeelezea kutokubali kamwe kuwepo kwa unyanyasaji ndani ya kanisa, maneno hayaendani na vitendo .

Kamati hiyo imekasirishwa zaidi na kwamba Utawala wa Vatcan unasisitiza kuwa unahusika zaidi na wahudumu wanaofanyika kazi ndani ya Vatcan kwenyewe , kuliko makasisi wake wanaofanyika kazi kwingineko duniani.
Mwezi Januari mwaka huu utawala wa Vatican ulichunguzwa upya na kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watoto, baada ya kupokea ukosoaji kama huo kwamba ulishindwa kuwalinda watoto waliokuwa chini ya uangalizi wake.

Wednesday, May 21, 2014

MIAKA 18 TOKA ILIPOZAMA MELI YA MV BUKOBA

Alfajiri ya Mei 21 mwaka 1996 ni siku itakayobaki kwenye kumbukumbu ya Watanzania baada ya watu zaidi ya 800 kufariki dunia kufuatia Meli ya MV Bukoba waliyokuwa wakisafiria kutoka mkoani Kagera kuelekea Mwanza kuzama katika Ziwa Victoria.
Tukiadhimisha miaka 18 tangu kutokea kwa ajali hiyo iliyokatisha maisha ya wapendwa wetu, taifa leo linakumbuka simanzi kutokana na kupoteza ndugu, uhai wa watu hao, ikiwemo mchango wao katika kuliletea taifa maendeleo.
Wakati ajali hiyo inatokea Rais Mstaafu  wa Awamu ya tatu BENJAMIN WILLIAM MKAPA alikuwa madarakani.
Ajali za majini zimeendelea kutokea ambapo Septemba 10 mwaka 2011 Meli ya Spice Islander ilizama katika eneo la Nungwi ikitokea Bandari ya Malindi Zanzibar na kuua zaidi ya watu 100.
Mwaka mmoja yaani Julai 18 2012, baadae karibu na Pwani ya Zanzibar Meli ya MV Skagit iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kwenda Zanzibar ilizama na kuua abiria 146 kati ya 290 waliokuwa kwenye meli hiyo.
Mara nyingi binadamu hujifunza kutokana na makosa, ambapo ajali hizi mara nyingi zinadaiwa kusababishwa na uzembe wa baadhi ya watendaji na watoa huduma
Aidha jamii imeitakiwa  kwa ujumla kuimarisha usalama katika usafiri wa majini na sio kuiachia mamlaka husika pekee.

SUALA LA ELIMU NI JUKUMU LA JAMII NZIMA - ABBAS KANDORO

Walimu na wadau wa elimu mkoani Mbeya wameitaka Serikali kutoa elimu kwa jamii juu ya mpango wa matokeo makubwa BRN ili mpango huo uweze kuleta tija.
Wakizungumza katika hafla ya kukabidhi vyeti kwa shule ambazo zimeongeza ufaulu kwenye mitihani ya kitaifa mkoani Mbeya, baadhi ya walimu wamesema bado kuna changamoto kubwa ya jamii kutoelewa malengo ya mpango huo,kiasi cha baadhi ya wazazi kutotoa ushirikiano katika maendeleo ya taaluma kwa watoto wao.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro amesema suala la maendeleo ya taaluma mkoani Mbeya ni jukumu la jamii nzima, hivyo ni muhimu kwa wazazi na walimu kushirikiana katika kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu  bora
Mkoa wa Mbeya ni miongoni mwa mikoa ambayo imefanya vizuri kitaaluma katika mwaka wa masomo wa 2013/2014 ukishika nafasi ya tatu katika mikoa yote ya Tanzania bara sambamba na kutoa shule iliyoongoza kitaifa kwenye matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2013.

JITIHADA ZA SERIKALI KUPAMBANA NA MIGOGORO YA WAFUGAJI NA WAKULIMA ZAANZA KUONESHA MAFANIKIO

Jitihada za Serikali na asasi za kiraia katika kuelimisha watu wa jamii ya ufugaji kutumia mifugo yao kupunguza umasikini, utunzaji wa mazingira na migogoro ya ardhi, zimeanza kuonesha mafanikio kwa baadhi ya maeneo hapa nchini.
Hali hiyo imebainika wilaya ya Manyoni mkoani Singida baada ya baadhi ya wafugaji katika eneo hilo, kuanza kuuza sehemu ya mifugo yao na kupata fedha zinazowasaidia kujenga makazi bora ya kuishi na kuwapatia elimu watoto wao.
Wakizungumza katika kijiji cha HEKA mara baada ya kutembelewa na katibu mkuu wa CCM ABDULRAHMAN KINANA, wafugaji hao wamesema hapo awali jamii hiyo ilikuwa nyuma kimaendeleo kwa kuwa hawakuelimishwa umuhimu wa kutumia mifugo katika kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wake katibu mkuu wa CCM komredi ABDULRAHMAN KINANA, amesema hatua hiyo imeonesha njia kwa wafugaji ambao wanajilimbikizia mifugo na kuwa watumwa wa mifugo yao.
Mkoa wa Singida una jumla ya wilaya tano na halmashauri zipatazo 6, huku asilimia 70 ya wananchi wake wakitegemea zaidi shughuli za kilimo na Ufugaji kwa ajili ya maendeleo yao.

KATIKA KUKABILIANA NA TATIZO LA MSONGAMANO WA MAGARI JIJINI DAR ES SALAAM SERIKALI YATENGA FUNGU MAALUM

Kwa muda mrefu jiji la Dar es Salaam limekuwa likikabiliwa na msongamano mkubwa wa magari yanayosababisha watu kuchelewa katika majukumu yao au kulazimika kuamka mapema kutokana na kutumia muda mwingi barabarani.
Kufuatia hali hiyo serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 28 elfu 945 nukta 00 kwa mwaka wa fedha 2014/2015 ili kukabiliana na changamoto hizo.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa Wizara ya Ujenzi Waziri wa Ujenzi Dk. JOHN POMBE MAGUFULI, amesema fedha hizo zitatumika kujenga barabara za mchepuo ambazo zitatumiwa kupunguza msongamano huo.
Kwa upande wa Kamati ya Miundombinu, mwakilishi wa kamati hiyo ABDALLAH MTUTURA ameitaka wizara ya ujenzi kutenga fedha nyingi za ndani kwa miradi ya barabara, huku Waziri kivuli wa Ujenzi FELIX MKOSAMALI akishauri kuanzishwa kwa wakala wa barabara za vijijini ili kuongeza usimamizi.
ZARINA MADABIDA mbunge wa viti maalum,MOSES MACHALI mbunge wa kasulu mjini, na ABDULKHARIM SHAA mbunge wa mafia, ni miongoni mwa wabunge waliochangia hoja ya bajeti ya wizara ya ujenzi.

ADAM PHILIP KUAMBIANA AZIKWA KATIKA MAKABURI YA KINONDONI JIJINI DAR ES SALAAM

MKE WA MAREHEMU ADAM KUAMBIANA, JANETH RITHE AKIWEKA SHADA LA MAUA KWENYE KABURI.
JB AKIWEKA SHADA LA MAUA
JB AKIINULIWA NA WASANII WENZAKE BAADA YA KUANGUKA KWA KUZIDIWA NA MACHUNGU WAKATI AKIZUNGUMZA

VILIO NA MAJONZI VYATAWALA KATIKA KUUAGA MWILI WA ADAM KUAMBIANA VIWANJA VYA LEADERS CLUB

PICHA YA ADAM PHILIP KUAMBIANA

WAOMBOLEZAJI WALIOFIKA KATIKA VIWANJA VYA LEADERS
STEVE NYERERE AKIELEKEZA WAGENI SEHEMU ZA KUKAA KATIKA VIWANJA VYA LEADERS
WAZIRI DKT. FENELLA MUKANGARA AKIWASILI KATIKA VIWANJA VYA LEADERS 
BAADHI YA WASANII WA FILMU WAKIWA KATIKA VIWANJA VYA LEADERS
WAANDISHI WA HABARI WAKICHUKUA MATUKIO MBALIMBALI
MSANII WA FILAMU "DOKII"
DKT. FENELLA MUKANGARA (KUSHOTO) AKIWA KATIKA VIWANJA VYA LEADERS


Tuesday, May 20, 2014

HII NDIO NYUMBA YA MILELE YA ADAM PHILIP KUAMBIANA

NYUMBA YA MILELE YA DIRECTOR NA MSANII WA FILAMU ADAM KUAMBIANA

VAN GAAL MENEJA MPYA WA MANCHESTER UNITED



Klabu ya Manchester United imemteua Lous Van Gaal kuwa kocha wake mpya atakayechukua nafasi baada ya David Moyes kutimuliwa kwa miezi 10 tu. Mholanzi huyo amesaini mkataba wa miaka mitatau na ataanza majukumu Old Trafford msimu unaokuja ikiwa ni baada kuongoza timu ya nchi yake Uholanzi katika kombe la dunia litakalofanyika nchini Brazil. Msaidi wa Van Gaal atakuwa Ryna Giggs mkongwe wa klabu hiyo ambayo alitwa majukumu ya kuiongoza Man U baada ya Moyes kufukuzwa zikiwa zimebaki mechi tatu msimu kukamilika. Van Gaal mwenye umri wa mika 62 amewahi kuzifundisha klabu za Ajax (Uholanzi), Barcelona (Uhispania) na Bayrn Munich (Ujerumani) ambazo aliziwezesha kushinda mataji ya Ligi Kuu kabla ya kuajiriwa kuiona kikosi cha taifa cha Uholanzi maarufu kama “Orange”.

Kocha huyo anategemewa kufufua matumaini ya United baada ya klabu hiyo kumaliza ya saba msimu huu chini ya Moyes na kuandikisha historia ya kuwa na msimu mbaya zaidi kwa kipindi cha miaka 24. Van Gaal alishinda mataji mawili ya La Liga akiwa na Barcelona na kujiunga na Bayern aliyotwaa nayo kombe la German Cup na kufika fainali Uefa. Alijizolea umaarufu mwaka 1995 baada ya kukiongoza kikosi kichanga cha Ajax kilichokuwa na Clarence Seadoff, Patrick Kluivert na wengine na kutwa kombe la Uefa kwa kuilaza AC Milan ya Italia.

UNAFAHAMU KILICHOMUA MSANII ADAM KUAMBIANA?

Mwili wa Adam Kuambiana ukipelekwa Hospitali ya Muhimbili.
KWELI kifo hakina huruma! Msemo huu umetimia juzi kufuatia kifo cha ghafla cha mwigizaji na mwongozaji wa filamu za Kibongo, Adam Philip Kuambiana (38) kilichotokea akiwa njiani kukimbizwa kwenye Hospitali ya Mama Ngoma, Mwenge jijini Dar es Salaam baada ya kuugua.

Kuambiana aliugua ghafla kwenye kambi ya kurekodi filamu na wasanii wenzake iliyopo katika Nyumba ya Kulala Wageni ya Silvarado iliyopo Sinza ya Kwaremmy, Dar.
NINI CHANZO CHA KIFO?
Akizungumza na Ijumaa Wikienda Jumamosi iliyopita nje ya Hospitali ya Mama Ngoma, msanii wa Bongo Fleva, Aboubakar Katwila ‘Q-Chillah’ alisema muda mchache kabla ya kufikwa na mauti,  Kuambiana alimlalamikia maumivu ya tumbo ambapo Ijumaa iliyopita alisema hali yake si nzuri kwani alikuwa akiendesha damu tupu.
Q-Chillah alisema: “Jana (Ijumaa) jioni Kuambiana na wasanii wenzake walikuwa baa wakinywa pombe hadi usiku mnene lakini bado aliendelea kulalamikia maumivu ya tumbo.
“Wenzake walimuuliza ni kwa nini alikuwa akiendelea kunywa pombe kama anaumwa? Akawaambia wamuache!
“Baada ya kumaliza kunywa kila mmoja alikwenda kulala chumbani kwake huku tukiahidiana kwamba itakapofika saa 3:00 asubuhi tuwe tayari kwa ajili ya kwenda ‘location’.
“Lakini ulipofika muda huo sisi tukiwa tayari kwa safari tulikwenda kugonga mlango wa chumba chake bila mafanikio.
“Cha kushangaza, alisikika sauti yake kwa mbali. Kwa bahati nzuri mlango ulikuwa wazi, mmoja akaingia ndani na kumkuta ameanguka chooni na hajiwezi. Neno lake la mwisho alisema kwamba anajisikia kuishiwa nguvu na anaharisha damu.
“Kutokana na hali yake hiyo mbaya tulimbeba na kumlaza kitandani kisha tukatafuta gari na kumkimbiza Hospitali ya Mama Ngoma ambapo daktari alisema kwamba alishafariki dunia muda mrefu.”

VIDONDA VYA TUMBO VYATAJWA
Kwa mujibu wa watu wa karibu, Kuambiana kwa muda mrefu amekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa vidonda vya tumbo (ulcers). Lakini pia inadaiwa alikuwa akisumbuliwa na kisukari (diabetes).
DAKTARI AELEZEA
Ijumaa Wikienda lilimtafuta daktari mmoja wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (aliomba jina kuhifadhiwa) ili azungumzie kuhusu vidonda vya tumbo, alisema:
“Kwa kawaida, mtu kuharisha damu kwa sababu ya vidonda vya tumbo inawezekana kabisa, hiyo kitaalam inaitwa heamatemesis. Inatokana na perforation ya tumbo yaani kidonda kuwa kikubwa.
“Kwa mtumiaji wa pombe ni kipindi anatakiwa kusimama au kuacha moja kwa moja. Kama hatajali afya yake anaweza kufa ghafla kwani uwezekano wa utumbo kukatika ghafla ni mkubwa.”
 ALIJUA KIFO CHAKE
Q-Chilla ambaye ni miongoni wa wasanii wanaocheza filamu hiyo, aliendelea kusema kuwa siku chache kabla ya kifo, Kuambiana alimwambia filamu yake hiyo inayoitwa Jojo ndiyo ya mwisho, hatajishughulisha tena na sanaa na alikuwa na mpango wa kwenda China kupumzika kwa muda mrefu.
Nimeumia sana kwani hii filamu ndiyo ilikuwa apate fedha nyingi sana kwa sababu ni ya kwake mwenyewe na ni kali mno, amecheza vizuri akinishirikisha mimi.
“Lakini ndiyo hivyo tena imeishia katikati, sijui ni nani atakayeiendeleza maana mwenyewe katuachia majonzi yasiyoelezeka,”alisema Q-Chillah.

AMEMFUATA MDOGO WAKE
Habari zaidi zinasema kwamba, Kuambiana ameaga dunia hata arobaini ya mdogo wake wa damu, Patrick  haijafika. Patrick alifariki dunia mwezi mmoja uliopita.
AKUTANA NA MHARIRI WA GLOBAL
Ijumaa saa 10:00 jioni maeneo ya Sinza Kwaremmy jirani na Silvarado, Kuambiana alikutana na Mhariri Kiongozi wa Magazeti Pendwa ya Global Publishers, Oscar Ndauka.
Mhariri huyo alimuuliza ni kwa nini hawaonani siku hizi, Kuambiana akajibu:
“Nipo Mr Ndauka, nipo bwana. Tutaonana lakini sina hakika sana.” Kuambiana alionekana mwenye afya njema na alimtania mhariri huyo kwa kumwambia: “Naona siku hizi Ndauka unazidi kunenepa tu, mi maisha yananipiga.”
Msanii wa Muziki wa Kizazi Kipya, Aboubakar Katwila ‘Q-Chillah’ na msanii aliyekuwa akishuti video  pamoja na Kuambiana muda mfupi kabla ya kifo wakiwa katika majonzi.

STEVE NYERERE, BATULI WALIA SANA
Baada ya taarifa kuenea, wasanii mbalimbali wa filamu walikusanyika katika Hospitali ya Mama Ngoma ambapo Mwenyekiti wa Bongo Movie Unity, Steven Mengere ‘Steve Nyerere’ na Yobnesh Yusuf ‘Batuli’ walivunja rekodi ya kulia kufuatia kifo hicho.

WADAU WAZUNGUMZIA MTU KUANGUKA CHOONI
Wadau na mashabiki wa filamu waliokuwa eneo hilo walisikika wakisema kwamba wasanii wengi hawana tabia za kucheki afya zao, jambo ambalo linawagharimu kiasi cha kupoteza maisha.
Wengine walisikika wakisema kwamba watu wanaoanguka chooni mara nyingi huwa hawaponi, wakipona huwa wanapooza miili.
“Unajua watu wengi wanakosea, pale mtu anapodondoka chooni wanamkimbiza hospitali badala ya kumtibu kienyeji, mtu akianguka  chooni tu anatakiwa kupewa ndizi mbivu lakini akipelekwa hospitali lazima afe,” walisikika watu.
HISTORIA YAKE KWA UFUPI
Marehemu Kuambiana alizaliwa mwaka 1976, Ifunda mkoani Iringa. Kabila ni Mmakua wa mkoani Mtwara.
Marehemu Kuambiana anatarajiwa kuzikwa leo Jumanne 20/5/2014 kwenye Makaburi ya Kinondoni jijini Dar.
Mungu ailaze pema peponi roho yake. Amina.
(Story na Picha kwa niaba ya Global Publishers)