Thursday, May 29, 2014

Al Sisi ashinda kwa kishindo uchaguzi wa rais Misri

Kiongozi wa zamani wa jeshi Abdel Fattah al Sisi ameibuka na ushindi mkubwa katika uchaguzi wa rais nchini Misri. Amejikingia zaidi ya asili mia 90 ya kura lakini walioteremka vituoni inasemekana ni asilimia 44 tu.

Kiongozi huyo zamani wa jeshi, kwa mujibu wa duru za sheria amepata asilimia 93 nukta 3 ya kura wakati shughuli za kuhesabu kura zikiwa tayari zimekamilika. Mgombea Hamdine Sabahi, mpinzani pekee katika uchaguzi huo amepata asilimia 3 nukta 8 ya kura, huku asilimia 3 nukta 7 ya kuwa ikiwa ni kura zilizoharibika.

Lakini idadi ya walioshiriki kupiga kura ikadiriwa asilimia 44 nukta 4, kwa mujibu wa duru hizo na hivyo kuweka shaka kwenye uhalali wa Al- Sisi, muasisi wa mapinduzi yaliyomuondowa madarakani Julai mwaka jana rais aliyechaguliwa kidemokrasia Mohamed Morsi.
Yalipoanza kutangazwa matokeo ya uchaguzi, wafuasi wa Al Sisi walizunguka barabara za Cairo na kupeperusha bendera wakisheherekea ushindi wa mgombea wao, huku honi za gari zikisikia katika mji mkuu.

Usiku kucha wafuasi hao wa Jemedari mstaafu Sisi walijumuika wakiimba na kucheza kwenye eneo maarufu la Tahrir lililoshuhudia maandamano makubwa yaliyompinduwa aliyekuwa rais wa Msri, Hosni Mubarak Novemba 2011, baada ya kuiongoza Misri kwa zaidi ya miaka 30.

No comments:

Post a Comment