Ili kukabiliana na uharamia na utekaji wa
mali za wavuvi unaofanywa kwenye ziwa Tanganyika, Mkuu wa mkoa wa Kigoma
ISSA MACHIBYA, ameitaka idara ya uhamiaji mkoani humo kuangalia upya taratibu
za utoaji wa vibali vya kazi ,na vibali vya kuishi, kwa watu kutoka nchi
za maziwa makuu ambao wanaajiriwa kufanya kazi za uvuvi mkoani Kigoma.
Akikabidhi mashine nne za boti ambazo
zimefanikiwa kuokolewa kutoka mikononi mwa majambazi kutoka Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo (DRC) mwanzoni mwa wiki hii, MACHIBYA amesema
uchunguzi unaonyesha kuwa vitendo
vya utekaji wa mali za wavuvi katika ziwa Tanganyika kwa kiasi kikubwa umekuwa
ukifanywa na watu kutoka nchi nchi hiyo na Burundi.
Kufuatia hali hiyo, mwenyekiti wa chama
cha wavuvi mkoani Kigoma RAMADHANI KANYONGO amesema, mali zenye thamani ya
zaidi ya shilingi bilioni tano zimeporwa mkoani humo, katika kipindi cha miaka
10 iliyopita.
Akitoa
taarifa kuhusu tukio lililotokea mwishoni mwa wiki iliyopita, Kamanda wa polisi
mkoa wa Kigoma FRAISSER KASHAI amesema, jumla ya boti moja na mashine saba za
boti zilitekwa, ambapo nahodha wa boti iliyotekwa alifanikiwa kuwatoroka
majambazi hayo kutoka mkoa wa KALEMIE nchini DRC na kufanikiwa kurudi na
mashine nne za boti ,ambazo zilikuwa sehemu ya vifaa vilivyotekwa katika tukio
hilo.
Kufuatia kitendo hicho cha kishujaa, mbali
na kumkabidhi fedha taslimu, Mkuu wa wilaya ya kibondo, VENANCE MWAMOTTO
Amemsifia nahodha huyo kwa kitendo chake
cha ujasiri.
No comments:
Post a Comment