Watendaji wa Halmashauri ya wilaya ya MBULU mkoani MANYARA wameagizwa kuhakikisha wanaweka
mipango mizuri ya matumizi bora ya Ardhi, ili kuepusha migogoro baina ya
WAFUGAJI na WAKULIMA inayosababisha wakati mwingine umwagikaji wa Damu.
Katibu mkuu wa
Chama cha Mapinduzi CCM, ABDULRAHMAN KINANA ametoa kauli hiyo, baada ya
kutembelea eneo la bonde la YAEDA wilayani humo, na kupata malalamiko ya
wananchi hao kuhusiana na mgogoro wa Ardhi kati ya WAFUGAJI, WAKULIMA na
WAWEKEZAJI, wanaodaiwa kudhulumu ardhi ya wanyonge katika eneo hilo.
Wakitoa
malalamiko hayo kwa katibu mkuu wa CCM, wananchi hao wamedai kuwepo
kwa kikundi cha watu kinachotumia mabavu na fedha, kuwaondoa
kutoka katika maeneo yao ya Asili kwa lengo la kutwaa ardhi ya wananchi
hao ambao wengi wao ni masikini.
Kufuatia
malalamiko hayo katibu mkuu wa CCM amekiri kuwa, migogoro mingi ya Ardhi
inayochukua sura mpya kila siku na umwagikaji wa damu kwa wasiokuwa na hatia,
inachangiwa zaidi na Watendaji wa Serikali kushindwa kutoa elimu kuhusu
matumizi bora ya Ardhi kwa Jamii za WAFUGAJI na WAKULIMA, huku mkuu wa wilaya
ya Mbulu ANATOLY CHOYA akielezea mikakati ya Serikali katika kukabiliana na
tatizo hilo.
Mkoa wa MANYARA
ni miongoni mwa maeneo yenye migogoro mingi ya Ardhi, inayochangia umasikini
kwa watu wake kwa kuwa wanatumia muda mwingi katika kushughulikia migogoro
hiyo, kuliko kufanya kazi za Maendeleo.
No comments:
Post a Comment