Thursday, May 29, 2014

Uchina Imeanza Kulegeza Sheria Zake Za Mpango Wa Uzazi

Uchina imeanza kulegeza sheria zake za mpango wa uzazi, na sasa inapiga kampeni ya kuongeza angalau watoto millioni mbili zaidi wanaozaliwa kila mwaka.
Serikali itaongeza wakunga na wahudumu sambamba na kupanua nafasi hospitalini na kuongezwa idadi ya vitanda na vifaa vinginevyo.
Kwa muda mrefu Uchina imeendeleza sera kali ya mpango wa uzazi ya kulazimu familia kuwa na mtoto mmoja tu, huku wanaokiuka wakichukuliwa hatua kali jambo linaloshutumiwa kimataifa.
Lakini mwaka jana serikali ilianza kulegeza kamba kwa kusema iwapo mmoja wa wazazi amekuwa mtoto wa pekee katika familia, basi anaweza kuzaa mtoto wa pili.
Japo hatua za awali zilichukuliwa kukabiliana na idadi kubwa ya watu nchini humo, sasa kumetokea mapungufu ambayo yanahitaji kusawazishwa.
Nao Wapanga sera wamependekeza juhudi hizo za kuongeza idadi ya watoto, zichukuliwe sasa la sivyo Uchina itajikuta na upungufu mkubwa wa nguvu kazi za vijana, huku idadi ya wazee na wanaostaafu ikiwa kubwa kiasi cha kuzorotesha uchumi wa taifa hilo kubwa duniani.

No comments:

Post a Comment