Monday, May 12, 2014

TANZANIA NI MIONGONI MWA NCHI ZINAZOATHIRIWA NA MABADILIKO YA TABIA NCHI

Mhe. Samia Suluhu Hassan
Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoathiriwa na mabadiliko ya tabianchi ambayo yamekuwa yakisababisha kuwepo kwa mvua nyingi pamoja na ukame katika baadhi ya maeneo.
Ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi, Waziri wa nchi ofisi ya makamu wa Rais Mazingira SAMIA SULUHU HASSAN,wakati akiwasilisha bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais kwa mwaka wa fedha 2014/2015,amesema wamepunguza gharama za nishati mbadala kwa asilimia 18 ya kodi ya ongezeko la thamani kwa vifaa vya uzalishaji wa nishati za upepo na gesi.
Kwa upande wa kamati ya Katiba, sheria na utawala, mwakilishi wa kamati hiyo FAHARIA SHOMARI, amesema wananchi wengi bado hawafahamu faida ya muungano na mgawanyo wa mapato huku mwakilishi wa kamati ya Maliasili na Mazingira ALSHAIMAA QWEGIR akiitaka Serikali kuvunja nyumba zote zilizojengwa kwenye hifadhi za mito, maziwa na bahari.
Katika hatua nyingine Kambi rasmi ya upinzani Bungeni kupitia kwa msemaji wake wa Katiba na Sheria TUNDU LISSU imehoji kutolewa kwa mapato pungufu kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kinyume na taratibu.
Tukisalia bungeni mbunge wa Kigamboni Dk. FAUSTIN NDUGULILE nae ameitaka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuwasilisha bungeni taarifa ya Ugonjwa wa Homa ya Dengu, Dalili zake na hatua zinazochukuliwa na Serikali mpaka sasa ili kuwatoa hofu wananchi jambo ambalo limeungwa mkono na Mwenyekiti wa Bunge MUSSA AZAN ZUNGU.

No comments:

Post a Comment