Siku moja baada ya kituo cha sheria na haki za
binaadamu LHRC, kuzindua ripoti ya taarifa kuhusu madhara kwa afya
na mazingira ya madini ya urani, baadhi ya wananchi wamesema hakuna
haja ya Serikali kusitisha uchimbaji wa madini hayo, badala yake ziwekwe njia
madhubuti za kudhibiti madhara.
Wakazi hao VEDASTO MKAKA, MAIMUNA IDDY, NA
ADNANI MITEMA wamesema, uzoefu unaonyesha kuwa sio Tanzania pekee
yenye madini kama hayo, hivyo kuacha kuyachimba kwa kuhofia madhara sio jambo
la msingi, na wametumia fursa hiyo kuwaomba wanaharakati hao kushirikiana na
serikali, kutafuta ufumbuzi wa hali hiyo.
Aidha akizungumza katika uzinduzi huo,
mkurugenzi wa kituo cha sheria na haki za binaadam Bi. HELEN KIJO
BISIMBA amesema, uzoefu wa kitaalamu kutoka katika nchi ambazo madini
hayo yanazalishwa unaonesha kuwa, zoezi la uchimbaji wa madini hayo linahitaji
kiwango kikubwa cha maji, huku athari kwa jamii kuhusu magonjwa ya ngozi
na kansa ikihofiwa kuwa kwa kiasi kikubwa.
Naye makamu mwenyekiti wa tume ya haki za
binadamu na utawala bora MAHAFUDHA HAMID amesema, uzoefu kutoka
katika machimbo mengi ya madini hapa nchini unaonesha kuwepo kwa baadhi ya
vitendo vya uvunjifu wa haki za binaadamu hivyo vyema sera ya madini ya urani
ikawekwa wazi kutokana na hatari iliyomo katika madini hayo, ili kuepusha
vitendo hivyo kutojitokeza.
Nayo baadhi ya Maeneo yaliyofanyiwa utafiti na
kubainika kuwa na madini ya urani ni Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma.
Miongoni mwa maeneo hapa nchini ambayo madini
ya urani yanategemewa kupatikana ni pamoja na NAMTUMBO, MANYONI na BAHI.
No comments:
Post a Comment