Wednesday, May 14, 2014

IDADI YA VIFO VYA KINA MAMA NA WATOTO CHINI UMRI WA 5 IMEZIDI KUSHIKA KASI

KATIBU MKUU WA CCM ABDULRAHMAN KINANA AKIWAHUTUBIA WANANCHI WA KATA YA ROYA WILAYA YA UYUI MKOANI TABORA
Imeelezwa kuwa ongezeko la idadi ya vifo vya akina mama wajawazito na watoto walio chini ya umri wa miaka 5 limezidi kushika kasi,  hususani katika maeneo ambayo hayafikiwi kiurahisi kutokana na miundo mbinu mibovu ya barabara na usafiri.
Kwa Tanzania hali hiyo imebainika katika kata ya ROYA wilaya ya UYUI mkoani TABORA, ambako wajawazito na watoto wadogo hawajawahi kupata chanjo,  za kujikinga na maradhi ya aina mbalimbali kwa zaidi ya miaka mitano.
Wananchi wa Kata hiyo wakizungumza mbele ya Katibu mkuu wa chama cha Mapinduzi CCM, komredi ABDULRAHMAN KINANA, wamedai hali hiyo imesababishwa na kukosekana kwa Jokofu la kuhifadhia dawa katika Zahanati ya kata hiyo.
Mara baada ya malalamiko hayo kutoka kwa wakazi wa kata hiyo, ikamlazimu katibu mkuu huyo wa CCM komredi KINANA kumtaka mbunge wa Jimbo hilo ATHUMANI MFUTAKAMBA, kujibu baadhi ya tuhuma hizo ingawa wananchi walionekana kutoridhishwa na majibu yake.
Hata hivyo kero hizo hazikuanzia hapo, ambapo awali katibu mkuu huyo alipofika katika kata ya MIYENZE wanachi katika eneo hilo ambao ni Jamii ya wafugaji wamelalamikia vitendo vya kikatili vinavyofanywa na askari wanyamapori vya kuua mifugo yao na kisha kuwakamata wamiliki wake. 
Kufuatia majibizano hayo Katibu mkuu wa CCM kwa mara nyingine tena ikamlazimu kuingilia kati na kutoa maelezo ya kina huku akiahidi kuifuatilia kero hiyo na kuitafutia ufumbuzi wa kudumu kulingana na mamlaka aliyopewa.
Wilaya ya Uyui kwa sasa ina jumla ya wakazi wanaofikia 393,789, huku ikiwa na ongezeko la idadi ya watu la wastani wa asilimia 4.8 kwa mwaka.

No comments:

Post a Comment