Mali imevituma vikosi kuukomboa mji wa Kaskazini mwa nchi hiyo Kidal,
kutoka mikononi mwa waasi wa Tuareg baada ya wafanyakazi 6 wa serikali
na raia 2 kuuawa, kufuatia shambulizi katika ofisi za Gavana wa jimbo
hil.
Waasi hao wa Tuareg pia wamewateka nyara watu 30. Shambulizi hilo
limemfanya Waziri Mkuu wa Mali Moussa Mara kutangaza vita dhidi ya
wanamgambo hao. Karibu wanajeshi wanane waliuawa huku wafanyakazi wa
umma 30 wakichukuliwa mateka na waasi baada ya mapigano kuzuka wakati wa
ziara ya Waziri Mkuu Moussa Mara katika mji huo wa kaskazini mwa Mali.
Msemaji wa waasi hao wanaopigania kujitenga amekanusha kuwa kuna yeyote
aliyeuawa ndani ya jengo hilo la serikali. Mara amewaambia waandishi wa
habari baada ya kuwasili Gao, mji mwingine wa Kaskazini, kuwa serikali
tayari imevituma vikosi vyake, wakiwemo wanajeshi maalum, kuukomboa mji
wa Kidal. Amesema magaidi wametangaza vita dhidi ya serikali, hivyo Mali
iko vitani na magaidi. Waziri wa Ulinzi wa Mali Soumeylou Boubeye Maiga
amesema wanajeshi wa serikali wamechukua udhibiti wa majengo yote ya
serikali, isipokuwa tu ofisi za gavana, ambazo bado zimeshikiliwa na
waasi.
Mara alikuwa akiuzuru mji huo, ambao ni ngome ya waasi wa Tuareg, kwa
mara ya kwanza tangu alipoteuliwa mwezi uliopita kama sehemu ya juhudi
za kuyafufua mazungumzo yaliyochelewa ya amani na makundi yenye silaha
kaskazini mwa nchi hiyo. Mara ameyakosoa majeshi ya Ufaransa na Umoja wa
Mataifa kwa kuliwacha shambulizi hilo kufanyika. Kikosi cha Kulinda
Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA, kimesema askari wake 21
walijeruhiwa katika mapambano hayo wakati wakiweka ulinzi kwa ziara
hiyo ya Waziri mkuu mjini Kidal. Haikubainika mara moja kama wanajeshi
wa Ufaransa walihusika katika matukio hayo ya mwishoni mwa wiki mjini
Kidal.
Marekani imetoa wito wa pande husika kujizuia na kuwachiliwa huru mara
moja kwa mateka hao. Imesema pande zote mbili zinastahili kutojihusisha
na vitendo vitakavyohatarisha maisha ya mwananchi wa kawaida. Wizara ya
Mambo ya Kigeni ya Marekani imesema njia pekee ya kupatikana amani ni
kupitia mazungumzo.
Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi – ECOWAS, yenye nchi 16
wanachama, pia imelaani machafuko hayo pamoja na “kuzorota pakubwa kwa
hali ya kisiasa na usalama”. Serikali ya Mali imesema vurugu hizo
zimesababishwa na waasi wa Tuareg wanaopigania kujitenga upande wa
mashariki mwa nchi, lakini Waziri Mkuu Mara amesema makundi ya
wanamgambo yanaitumia fursa ya mzozo uliopo ili kujipenyeza mjini Kidal,
ili kushiriki katika machafuko hayo pamoja na makundi mengine ya
kigaidi.
Baada ya kurejea mjini Bamako jana usiku, Mara amesema maafisa
wanaendelea na juhudi za kuwezesha kuwachiliwa huru mateka hao. Amesema
wengine “wameuawa kinyama, huku wengine wakiwachiwa huru kwa sababu ya
majeraha waliyoyapata katika makabiliano hayo.
No comments:
Post a Comment